Kiungo kutoka nchini Rwanda Haruna Niyonzima huenda akarudi Tanzania na kucheza tena Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, huku ikielezwa atajiunga na Geita Gold FC.
Geita Gold FC inatarajia kutumia mwanya wa Dirisha Dogo la Usajili litakalofunguliwa rasmi Desemba 15, kukiimarisha kikosi chao kwa ajili ya Mshike Mshike wa Ligi Kuu msimu huu 2021/22.
Niyonzima ambaye kwa sasa anaitumikia klabu ya AS Kigali ya nchini kwao Rwanda anatajwa huenda akawasili Tanzania mwishoni mwa juma hili, ili kumalizana na Uongozi wa Geita Gold.
Taarifa zinaeleza kuwa Niyonzima atasaini mkataba wa mwaka mmoja, na atajiunga moja kwa moja na kikosi cha klabu hiyo baada ya kuwasili nchini.
Kabla ya kurejea nchini kwao Rwanda Niyonzima aliwahi kuitumikia Young Africana na Simba SC kwa vipindi tofauti, huku akitwaa taji la Tanzania bara akiwa na miamba hiyo ya Soka ya Jijini Dar es salaam.