Shirikisho la Soka Duniani ‘FIFA’ limeifungia kwa muda klabu ya Geita Gold FC kufanya usajili wa wachezaji kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu 2022/23, hadi itakapomlipa stahiki zake Kocha Etiene Ndayiragije.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’, Geita Gold FC haitaruhusiwa kufanya usajili wa wachezaji nje na ndani ya nchi, mpaka itakapomlipa Kocha huyo raia wa Burundi.
Taarifa hiyo imeendelea kueleza kuwa, FIFA umesema endapo Klabu ya Geita Gold itashindwa kumlipa Kocha huyo kwa wakati, suala hilo litawasilishwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho hilo kwa hatua zaidi za Kinidhamu.
Ndayiragije aliajiriwa Geita Gold FC mwanzoni mwa msimu huu 2021/22, lakini kibarua chake kilisitishwa kufuatia mwenendo wa kikosi cha klabu hiyo kutoridhisha, na aliyekuwa msaidizi wake Fred Felix Minziro alikabidhiwa mikoba ya kuwa Kocha Mkuu.
Geita Gold FC kwa sasa ipo nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa na kila sababu ya kumaliza katika nafasi hiyo ama ya tatu, kutokana na mwenendo mzuri walio nao katika kipindi hiki cha kuelekea mwishoni mwa msimu.
Kama itamaliza nafasi ya tatu ama ya nne, itapata wasaa wa kuiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu ujao 2022/23.