Saa chache baada ya Simba SC kutua jijini Mwanza tayari kwa mchezo wa Mzunguuko wa 16 wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kocha msaidizi wa timu ya Geita Gold FC, Mathias Wadiba, amesema hawana hofu na mchezo huo.
Mapema leo Ijumaa (Desemba 16) Simba SC iliwasili jijini Mwanza ikitokea Dar es salaam, kwa mchezo huo utakaopigwa Jumapili (Desemba 18) katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Kocha Wadiba amesema kikosi cha Geita Gold FC kimejiandaa vizuri kuikabili Simba SC kwenye mchezo huo, na wana imani mambo yatawanyokea na kupata alama tatu za mchezo huo.
Amesema kinachowafanya kutokua na hosfu na mchezo huo, ni kuamini Simba SC ni timu ya kawaida kwa sababu wote wapo Daraja moja, wakicheza Ligi Kuu pamoja na kwamba wanawaheshimu.
“Tunawaheshimu Simba SC, lakini hatuna hofu nao kwa kuwa wote tunacheza Ligi moja, tumejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo huo na tunaamini kuwa tutafanya vizuri,” amesema kocha huyo.
Wakati Simba SC ikiwa nafasi ya tatu kwa kumiliki alama 34, lakini ikiwa vinara wa kufunga mabao baada ya kufunga 31, lakini ikiwa pia inashika nafasi ya kwanza kwa kufungwa mabao machache baada ya kuruhusu saba tu huku Geita ikiwa nafasi ya tano baada ya kukusanya alama 22 kwenye michezo 35.
Huu unatajwa kuwa mmoja kati ya michezo mizuri kutokana na upinzani ambao Simba SC imekuwa ikikutana nao kila inapokwenda ugenini kwenye michezo ya Ligi Kuu.