Mkuu wa Idara ya Habari ya Geita Gold, Samwel Didda amesema kuwa mipango iliyopo kwa sasa ni kupata ushindi kwenye mechi zilizobaki ikiwa ni pamoja na mchezo dhidi ya Mbeya City.
Geita Gold FC itaikaribisha Mbeya City FC katika Uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita Mei 13, huku kila upande ukizihitaji alama tatu za mchezo huo ili kujiimarisha katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Ikumbukwe kuwa michezo yao iliyopita wote walifungwa ambapo Geita Gold ilikubali kupoteza kwa kufungwa 1-3 dhidi ya Tanzania Prisons, huku MBeya City ikifungwa na Kagera Sugar 0-1.
Didda amesema kuwa baada ya kupoteza dhidi ya Tanzania Prisons, kikosi chao kilianza maandalizi kwa ajili ya mchezo dhidi ya Mbeya City na hali ya kambi ipo vizuri kwa ajili ya kuzinasa alama tatu muhimu.
“Mchezo utakuwa mgumu sana maana kila timu imetoka kupoteza lazima tufanye kazi kubwa kupata matokeo, kuna makosa ambayo yapo tutafanyia kazi.”
“Mashabiki wajitokeze kwa wingi kuja kuangalia burudani ya kutosha na tunaimani tutapata alama tatu katika mchezo huo.” Amesema Didda