Mkuu wa wilaya ya Geita, Jesephat Maganga ameagiza idara ya udhibiti ubora wa elimu halmashauri ya Geita kuchunguza uhamisho wa walimu, baada ya kuibuka madai kuwa ni moja ya sababu za matokeo mabaya ya darasa la saba mwaka huu.
Akizungumza wakti wa kikao cha wadau wa elimu, Maganga ameagiza uchunguzi huo uhusishe kufahamu idadi ya walimu waliohamishwa na kiwango cha fedha za uhamisho walicholipwa.
“Kuna kitu kimejificha nyuma ya huu uhamisho wa walimu na kiasi cha fedha zinazotumika kugharamia uhamisho huo, tuchunguze kwa makini kubaini ukweli” amesema Maganga.
Halmashauri ya Geita yenyeshule 196 za msingi imeshika mkia kwa ufaulu kati ya halmashauri sita za mkoa huo.
Awali, Ofisa elimu kata ya Isulwabutundwe, Fortunatus Kezilahabi alisema uhamisho wa walimu usiozingatia ikama umeifanya kata yake kuwa na idadi ndogo ya walimu kulinganisha na mahitaji.
“Mwaka mmoja kata ya Isulwabutundwe imepoteza walimu 21, wanne wamepandishwa vyeo, 16 walihamishwa na mmoja amefukuzwa. walimu sita walihamishwa shule moja kwa wakati mmoja bila nafasi zao kujazwa” amesisitiza Kezilahabi.