Mshambuliaji wa pembeni kutoka nchini Ureno Gelson Martins, amejiunga na klabu ya Atletico Madrid akitokea Sporting Lisbon, baada ya kumaliza mkataba wake mwezi uliopita.
Martins amejiunga na klabu hiyo ya mjini Madrid kama mchezji huru, na leo jumatano amethibitisha rasmi kuwa mchezaji wa halali wa kikosi cha Atletico kinachonolewa meneja kutoka Argentina Diego Simione.
“Klabu yetu imefikia makubaliano ya kumsajili Gelson Martins, anakua mchezaji mpya aliyesajiliwa katika kipindi hiki cha dirisha la usajili wa majira ya kiangazi,” imeeleza taarifa iliyotolewa na uongozi wa Atletico Madrid.
“Mshambuliaji huyu kutoka Ureno amesaini mkataba wa miaka sita wa kuitumikia klabu yetu, amejiunga nasi akiwa mchezaji huru.”
Martins ameondoka Sporting Lisbon, huku akiacha kumbukumbu ya kuwa sehemu ya kikosi cha klabu hiyo kilichomaliza katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ya Ureno msimu uliopita, pamoja na kufika hatua ya robo fainali ya michuano ya Europa League.
Martins ameshaitumikia timu ya taifa ya Ureno mara 19, na alikua sehemu ya kikosi cha timu hiyo wakati wa fainali za kombe la dunia zilizomalizika nchini Urusi Julai 15. Alicheza mchezo wa mzunguko wa pili hatua ya makundi dhidi ya Morocco ambao walikubali kufungwa bao moja kwa sifuri.
Martins mwenye umri wa miaka 23, anakua mchezaji wa tano kusajili wa na klabu ya Atletico katika kipindi hiki, akitanguliwa na Thomas Lemar akitokea AS Monaco, Rodri (Villarreal), Jonny Castro (Celta Vigo) pamoja na Antonio Adan kutoka Real Betis.