Mshambuliaji wa FC Lupopo, Mtanzania George Mpole anautazamia msimu ujao kufanya makubwa kwenye Ligi Kuu ya Congo, baada ya ligi iliyopita kufutwa, hivyo hakupata muda mzuri wa kucheza kama ilivyokuwa matarajio yake.
Tayari Mpole amejiunga na timu na amethibitisha kwamba ligi hiyo itaanza mwezi ujao, hivyo anajipanga kuhakikisha anafanya kazi nzuri na anaipeperusha vyema bendara ya Tanzania kwa kuonyesha kiwango cha juu.
“Msimu uliopita kwangu ulikuwa na changamoto mbili ya kwanza nisingeweza kucheza michuano ya CAF kwa sababu tayari nilicheza nikiwa na Geita Gold, jambo la pili ligi ikafutwa hivyo nikajikuta sijafanya kile nilichokitarajia.
“Najua kikosi chetu kina ushindani, pia wanasubiri kwa hamu kuona nitafanya nini, maana wakati natambulishwa kwa mara ya kwanza wachezaji wenzangu walifurahia kutokana na rekodi ya mabao 17 niliyoyafunga Geita.”
Amesema bado hajajua ligi ya Kongo ni ya aina gani, isipokuwa anapata elimu kupitia wachezaji wenzake na namna alivyowaona wakicheza michuano ya CAF akaona inahitaji ufiti wa mazoezi.
“Kabla ya kurejea kwenye timu, nilitumia muda wangu wa mapumziko kufanya mazoezi ili kujiweka sawa, hilo litanisaidia kutoanza moja kufanya maandalizi ya msimu ujao,” amesema