Mtanzania anayesukuma Kabumbu katika klabu ya FC Lupopo ya DR Congo George Mpole amezipongeza Klabu za Simba SC na Young Africans, kwa kutinga hatua ya Robo Fainali katika Michuano ya Kimataifa ( Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Barani Afrika).
Simba SC juzi Jumamosi (Machi 18) ilijihakikishia kutinga Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa kuifunga Horoya AC ya Guinea 7-0, huku Young Africans ikifanya hivyo kwakuichapa US Monastir ya Tunisia 2-0 jana Jumapili (Machi 19).
Mpole amesema mafanikio ya Simba SC na Young Africans yameifanya Tanzania iendelee kutoa timu nne kwenye mashindano ya kimataifa kutokana na alama walizozikusanya zisizoweza kufikiwa na nchi nyingine yeyote na hiyo ni heshima kubwa kwa taifa.
Mpole amesema ni wakati wa serikali kuiangalia kwa jicho la karibu timu hizo katika hatua hiyo ili kuzipa motisha zaidi na wao kuendeleza ubora kwenye mashindano hayo.
“Simba SC na Young Africans zinahitajika kutazamwa kwa jicho la pili zimekuwa timu bora zinayolifanya soka la Tanzania kuwa bora na kuwavutia mastaa mbalimbali kutoka nje kutamani kuja kucheza ligi yetu.”
“Walichokifanya kwenye hatua ya makundi ni kitu sahihi kiliongeza ushindani kwa wachezaji wenyewe kwa wenyewe na timu kuweza kufikia lengo hilo linatakiwa kuendelezwa hatua inayofuata ikiwezekana kwa kuongeza dau ambalo litatoa chachu”
“Ubora wa Simba SC kwenye mashindano ya kimataifa umeifanya Yanga pia kujitafakari na wao kujipanga na kufanya vyema tofauti na misimu ya nyuma pia wametinga hatua hiyo, hivyo wanahitaji motisha zaidi ili kuendelea kukuza soka la Afrika,” amesema Mpole aliyefunga mabao 17 na kubeba kiatu msimu uliopita akiwa na Geita Gold FC.