Mshambuliaji wa Geita Gold FC George Mpole ameahidi kuendelea kufunga akiwa na kikosi cha timu ya taifa ‘Taifa Stars’ endapo Kocha Mkuu Kim Poulsen atampa nafasi.
Mpole aliifungia Stars bao la mapema jana Jumamosi (Juni 04) katika mchezo wa kwanza wa Kundi F wa kuwania tiketi ya kucheza AFVON 2023, dhidi ya Niger iliyokuwa nyumbani Uwanja wa Taifa wa Benin.
Mpole ametangaza uhakika wa kuendelea kuwafurahisha watanzania, baada ya kuwasili jijini Dar es salaam mapema leo Jumapili (Juni 05) sambamba na wachezaji wenzake wakitokea Benin, ambako walicheza dhidi ya Niger.
Amesema kazi yake kama mshambuliaji ni kufunga na ataendelea kufanya hivyo, endapo Kocha Paulsen atampa nafasi ya kucheza, kama.ilivyokua katika mchezo wa jana Jumamosi.
“Jukumu langu ni kuhakikisha ninaifungia timu mabao, nitaendelea kufanya hivyo kama kocha atanipa nafasi ya kucheza kama ilivyokua jana.”
“Najua watanzania wanahitaji nini kutoka kwetu, tutapambana kwa ajili yao kwa sababu sisi ndio wawakilishi wao pale uwanjani, hivyo nikibebeshwa jukumu la kucheza nafasi ya ushambuliaji nitawapambania ili nifunge.” amesema Mpole
Stars itacheza mchezo wa pili wa kusaka tiketi ya AFCON 2023 Jumatano (Juni 08) dhidi ya Algaria, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Msimamo wa Kundi F baada ya mzunguuko wa kwanza unaonyesha Algeria iliyoibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Uganda jana Jumamosi, inaongoza kwa alama 03, Tanzania na Niger zina alama 01 na The Cranes inaburuza mkia.