Mshindi pekee wa tuzo ya Ballon d’Or kutoka Afrika, George Weah amejitosa kwa mara nyingine kwenye kinyang’anyiro cha urais wa Liberia utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Weah ambaye ni Seneta nchini humo na mwanaharakati wa haki za binadamu ametangaza kuwania nafasi hiyo ya juu zaidi kwa tiketi ya Democratic Change (CDC) akishirikiana na Jewel Howard –Taylor ambaye ni mke wa zamani wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Charles Taylor. Mama Taylor atakuwa mgombea mwenza wa George Weah na endapo watashinda atakuwa makamu wa Rais.

Weah amesema kuwa wakati huu yuko tayari zaidi kuwa Rais wa Liberia baada ya kushindwa katika uchaguzi uliofanyika mwaka 2005.

“Niko tayari kwa asilimia mia moja kuchukua Urais wakati huu,” Weah anakaririwa na vyombo vya habari vya Liberia.

Weah ni mtu maarufu zaidi Liberia akiwa na historia ya kulitangaza taifa hilo kupitia soka miaka ya 1990, akishinda tuzo ya Ballon d’Or mwaka 1995 huku akibeba tuzo ya uchezaji bora wa Afrika mara tatu.

Mwaka 1995, Weah alitajwa kuwa mchezaji bora wa Afrika wa Karne na mwaka 2004 alitajwa kwenye orodha ya wachezaji 100 bora zaidi duniani wanaoishi.

Hata hivyo, kwa sheria za nchi hiyo na sheria za kimataifa zinafanya nafasi ya urais kuwa kaa la moto, kwani aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Charles Taylor anatumikia kifungo cha miaka 50 jela kwa kosa la kuchochea vita ya kisiasa nchini Sierra Leone.

Barcelona kuishtaki PSG, wahofia walikotoa fedha kumnasa Neymar
Polepole azipita kando hoja za Chadema kuhusu hali ya Uchumi