Rais wa Liberia na aliyekua nahodha wa timu ya taifa ya nchi hiyo, George Weah usiku wa kuamkia leo aliwashangaza wananchi wake kwa kurejea uwanjani na kusakatata kabumbu, wakati wa mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Nigeria uliochezwa mjini Monrovia.

Weah ambaye aliwahi kuwa mchezaji bora wa dunia mwaka 1995, alicheza sehemu ya mchezo huo, ambao ulimalizika kwa Liberia kukubalia kufungwa mabao mawili kwa moja.

Shirikisho la soka nchini Liberia liliandaa mchezo huo wa kimataifa wa kirafiki kwa lengo la kuistaafisha jezi namba 14 ya timu ya taifa, ambayo ilikua ikitumiwa na rais huyo, ambaye siku chache zilizopita alitimiza umri wa miaka 52.

Katika kuhakikisha shughuli ya kustaafishwa kwa jezi hiyo inatimia, Rais Weah alilazimika kucheza huku akiwa amevaa namna 14 mgongoni, jambo ambalo lilionyesha kuwafurahisha mashabiki wa soka nchini Liberia ambao hawakubahatika kumuona wakati akicheza soka la ushindani.

Kama ilivyokua kawaida yake, Weah alicheza nafasi ya ushambuliaji baada ya kuingia uwanjani dakika ya 72, huku mashabiki waliokua wamefurika uwanjani hapo wakisimama na kumpa heshima.

Mabao ya Nigeria katika mchezo huo yalifungwa na Henry Onyekuru na Simeon Nwankwo huku bao la kufutia machozi la Liberia, likifungwa na mshambiliaji wa zamani wa Young Africans ya Tanzania Kpah Sherman kwa mkwaju wa penati.

Wakati akicheza soka Weah alitamba sana katika bara la Ulaya akiwa na klabu za AS Monaco, Paris Saint-Germain na Marseille zote za Ufaransa, AC Milan ya Italia, Manchester City na Chelsea za England.

Bado anaendelea kushikilia rekodi ya kuwa mwafrika pekee aliyewahi kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa dunia.

Video: Maalim Seif avutwa Chadema, Mwamunyange atema cheche
Msanii aomba aendelee kufungwa kwa kujaribu kumuua Rais Kagame