Baada ya kupokea kisago cha 2-1 kutoka kwa Deportivo La Coruna, beki wa kati wa FC Barcelona, Gerard Pique amewajibu mashabiki wanaotoa lawama kufuatia kipigo hicho.
Pique ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha Barca katika mchezo huo uliounguruma Estadio Riazor, aliwaambia waandishi wa habari kuwa anashangazwa na baadhi ya mashabiki kuwatupia lawama wao kama wachezaji.
Pique alisema ni upumbavu na ujinga kulaumu baada ya kufungwa, kwani haimuingii akilini kwa mashabiki hao kuamini wachezaji wa klabu yao hawawezi kufungwa kwa kuhisi ni wao maroboti ambayo hufanya kazi bila kuchoka.
Alisema wachezaji wa Barcelona ni binaadamu kama binadamu wengine na ni wachezaji kama ilivyo kwa klabu nyingine. Hivyo, lipotokea jambo la kupoteza mchezo wanatakia kuchukuliwa hivyo na sio kama wanafikiriwa hivi sasa.
“Tulifanya kazi kubwa katikati ya juma, tumefanikiwa kupitia katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya kwa kupata ushindi wa mabao sita kwa moja dhidi ya timu ngumu ya PSG, kufungwa na Deportivo La Coruna isichukuliwe kama tumefanya kusudi,” alisema.
“Hakuna anaependa kufungwa, hili limetokea kama linavyotokea kwa wengine, sisi ni binaadamu, sio maroboti ambayo yanaweza kufanya kazi bila kuchoka,” Pique aliongeza.
Kufungwa kwa FC Barcelona, kumeiporomosha klabu hiyo ya mjini Barcelona hadi katika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi ya Hispania, kufuatia mahasimu wao Real Madrid kuchomoza na ushindi wa mabao mawili kwa moja dhidi ya Real Betis.
Mabao ya Deportivo yalifungwa na Joselu Depor na Alex Bergantinos huku Luis Suarez akifunga bao la kuwafuta machozi wachezaji wenzake wa FC Barcelona.