Gereza maarufu kwa kuwashikilia wafungwa wa kisiasa na waandishi wa habari pamoja na wanaharakati nchini Ethiopia limefungwa rasmi wiki hii, baada ya nchi hiyo kumpata Waziri Mkuu mpya.
Hatua hiyo ya kulifunga gereza hilo maarufu la Oromia imekuja wakati ambapo maandamano ya kuipinga Serikali yameendelea kukoma. Hiyo ni moja kati ya hatua zilizochukuliwa kurejesha hali ya utulivu nchini humo.
Wafungwa watahamishiwa kwenye magereza mengine nchini humo.
Waziri Mkuu mpya, Abiy Ahmed ameahidi kufanya kila linalowezekana kurekebisha makosa yaliyofanywa na Serikali na kutimiza kwa kiasi kikubwa mahitaji ya wananchi walioamua kuingia barabarani kupinga utawala uliokuwa madarakani.
Nchi hiyo ilikubwa na maandamano makubwa kwa miezi kadhaa mfululizo, yanayotajwa kuwa ni moja kati ya maandamano makubwa zaidi ya kuipinga Serikali katika robo karne iliyopita.
Waandamanaji waliojikusanya kupitia mitandao ya kijamii walikuwa wakidai uhuru zaidi katika masuala mbalimbali.
Maandamano yalianzia katika mikoa ya Oromia na Amhara mwishoni mwa mwaka 2015 na baadaye kusambaa katika maeneo mengine yakisababisha biashara nyingi kufungwa pamoja na miundombinu ya usafiri.
Hatua hiyo ilisababisha Serikali kutangaza hali ya dharura nchini humo miezi michache iliyopita, baada ya maandamano kufikia kilele chake na kutishia zaidi hali ya amani.
Wakaazi wa Oromia wameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa wamerejeshewa huduma za mtandao zilizokuwa zimezimwa ili kuepusha watu kuhamasishana kuandamana kupitia mitandao ya kijamii.