Msemaji Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Gerson Msigwa amesema Tanzania inahitaji kuleta Teknolojia ya usaidizi wa video itakayowawezesha Waamuzi kuona matukio tata ambayo kwa sasa yamekuwa yakiwaweka matatani wanapochezesha Michezo ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’.
Mjadala wa Teknolojia hiyo inayotumika kwenye ligi kubwa za barani Ulaya na Michuano ya Kimataifa uliibuliwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mwigulu Nchemba mapema mwaka huu 2022, kufuatia matukio tata yaliyojitokeza katika baadhi ya michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Msigwa amesema ni wazi Serikali imeyasikia malalamiko mengi yanayohusisha maamuzi yenye mkanganyiko kwenye michezo ya Ligi Kuu jambo ambalo hayawafurahishi wao wakiwa ni wadau namba moja ya mchezo huo.
”Kwa hali ilivyo sasa na Teknolojia ilipofika hatuna namna tunaweza kuiepuka VAR, inawezekana tusiwenayo leo kwa sababu uwekezaji wake ni gharama kubwa sana, lakini ni kitu ambacho tunakihitaji, tunajua Waziri wa fedha ni mwanamichezo na angependa hizi dosari tuziondoe kwa kutumia VAR”
“Hata mimi ni mwanamichezo nisingependa ziendelee kuwepo ,kwa hivyo ni dhamira ya Serikali baadaye tunakokwenda huko kadri ya uwezo wetu ili tuwe na VAR, ili kuondoa haya malalamiko ya magoli ya mkono, goli sio goli, penati sio penati, kashika hajashika,” amesema Gerson Msigwa Msemaji Mkuu wa Serikali.
Barani Afrika kwa sasa nchi ya Morocco pekee ndiyo yenye mfumo wa VAR unaotumika kwenye Ligi Kuu ya nchini humo.
VAR kwa sasa inatumika kwenye ligi zaidi ya 50 duniani kote, sambamba na Michuano inayoratibiwa na Shirikisho la Soka Duniani ‘FIFA’.