Mamlaka za usalama nchini Uturuki, zimesema mripuko wa geri aina ya metani ndiyo chanzo cha maafa yaliyotokea katika mgodi wa makaa ya mawe wa Bartin, uliopo kaskazini mwa nchi hiyo, ambapo idadi ya walifariki imefikia watu 41 na shughuli za uokozi bado zinaendelea.
Waziri wa mambo ya ndani wa Uturuki, Suleyman Soylu amesema wakati wa mlipuko watu 110 walikuwa ndani ya mgodi huo, na kwamba watu 58 miongoni mwao walikuwa tayari wameokolewa wakiwa salama mara baada ya kufika katika mgodi huo.
Amesema, ”Bado moto unawaka mgodini, wachimbaji pamoja na waokoaji wamejitolea pakubwa kuhakikisha hakuna ndugu yao anayeachwa nyuma, wachimbamigodi 10 wanaendelea kupata matibabu katika hospitali za Bartin na Istanbul, na mmoja tayari ameruhusiwa kurudi nyumbani.
Habari za mwanzo kuhusu walionaswa mgodini zilitolewa na wenzao walioweza kukimbia haraka na kutoka nje na tayari Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan aliyetarajiwa kusafiri kwa ndege kuzuru eneo la ajali hapo jana (Oktoba 15, 2022), kupitia ukurasa wake wa twitter ameandika kuwa uchunguzi wa kina utafanyika kubainisha kilichotokea.
Awali, Waziri wa nishati wa nchi hiyo, Fatih Donmez alisema kuwa sehemu kubwa moto uliozuka mgodini hapo, ulikuwa umedhibitiwa huku juhudi za kupoza eneo ulipotokea moto huo, kiasi cha mita 350 chini ya ardhi, zikiendelea.
Kwa upande wake Meya wa Amsara, Recai Cakir alibainisha kuwa wafanyakazi wa uokozi wapatao 70 walikuwa wameweza kufika kwenye chanzo cha mripuko, katika kina cha mita zipatazo 250 chini ya ardhi huku Mamlaka za Usalama zikisema kuwa waendesha mashtaka wameanzisha uchunguzi kujua chanzo cha moto huo.
Hata hivyo, shirikisho la huduma za kushughulikia majanga nchini Uturuki (AFAD), lilikuwa limearifu kuwa moto huo ulianzishwa na cheche kwenye transfoma ambayo ilikuwa imekumbwa na hitilafu, lakini baadaye limeiondoa dhana hiyo, likiafikiana na ile ya mrundikano wa gesi ya metani.
Itakumbukwa mwaka 2014, wafanyakazi 301 walifariki katika ajali mbaya ya mgodini nchini Uturuki, ambayo ilitokea katika mji wa Soma ulio umbali wa kilomita 350 kusini mwa jiji la nchi hiyo Istanbul.