Kampuni ya Geita Gold Mining Limited – GGML, imetoa msaada wa vifaa tiba wenye thamani ya Shilingi 260 milioni kwa Halmashauri ya Wilaya na Halmashauri ya Mji wa Geita, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuendelea kuboresha Sekta ya Afya Mkoani Geita,
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo jana mkoani Geita, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Kanali Boniphace Maghembe aliishukuru GGML kwa kuithamini jamii inayozunguka migodi na kusema wamekuwa wakishirikiana na Serikali kutekeleza miradi kadhaa ya afya hususan ujenzi wa zahanati na vituo vya afya.
Msaada huo , unajumuisha vitanda 17 vya Hospitali, Vitanda vitano vya uchunguzi wa Kitabibu, Majokofu maalumu ya kukusanya Damu na Magodoro ambapo pia imetoa vifaa maalumu vya uchunguzi wa via vya uzazi kwa mwanamke, viua wadudu, majokofu ya kuhifadhia maiti, vifaa vya upasuaji, mashine za kufulia na darubini.
Meneja Mwandamizi anayesimamia mahusiano endelevu ya kijamii kutoka GGML, Gilbert Mworia alisisitiza umuhimu wa huduma bora za afya katika kufikia lengo la 3 la Umoja wa Mataifa la Maendeleo Endelevu, ambalo linalenga katika kuhakikisha maisha ya afya na kukuza ustawi kwa wote.
Alisema, “Lengo la 3 la Maendeleo Endelevu ni miongoni mwa Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2015, na GGML imejidhatiti katika kuboresha afya na ustawi wa watu, imeboresha upatikanaji wa huduma bora za afya mkoani Geita si tu kwa msaada wa vifaa tiba, bali pia kupitia ujenzi wa Zahanati na vituo vya afya.”
Tangu kuanzishwa kwake mwaka wa 2000, GGML imejitolea kuboresha ustawi wa jamii inayozunguka mgodi kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa ikiwamo afya, elimu, maji, barabara na miradi ya kiuchumi.