JUMLA ya wahitimu 50 wa vyuo vikuu nchini, wamepata mafunzo yanayotolewa na Kampuni ya Geita Gold Mining Ltd (GGML), ya fani mbalimbali ndani ya idara hiyo kwa lengo la kuwezesha kupata uzoefu na kuwa na sifa za kuajiriwa.
Akizungumza katika hafla ya kuwakaribisha wahitimu hao mjini Geita, Mkurugenzi Mkuu wa GGML, Terry Strong alisema kupitia Mpango wa Mafunzo kazini, kampuni hiyo imekuwa mdau wa kuunga mkono mipango ya serikali, ya kuimarisha uwezo wa wahitimu kuajiriwa nchini baada ya kutekeleza mafunzo ya kazi na programu nyingine za wahitimu.
Amesema, “Programu ya mafunzo hayo inatekelezwa kwa kipindi cha miezi 12 na mwaka huu GGML imetoa nafasi za mafunzo kwa wahitimu 50 kati yao wanawake 30 na wanaume 20. Tungependa kuwatakia kila la heri wanaporipoti leo kwa idara zao tofauti,” alisema.
Kwa upande wake, Meneja Mwandamizi wa Afya, Usalama, Mazingira na Mafunzo wa GGML, Dkt. Kiva Mvungi, amewapongeza wahitimu waliojiunga na GGML na kuwaonya kuwa makini na matapeli wa ajira.
“Jihadharini na matapeli! GGML haipokei pesa ili upate kazi au fursa nyingine yoyote ndani ya kampuni. Iwapo utaombwa pesa ili upate ofa ya kazi au unashuku jambo kama hilo, tafadhali ripoti hili mara moja kwa Idara yetu ya Usalama, Kitengo cha Upelelezi, kwa kupiga simu +255 756 808 128 / +255 28 216 01 40 Ext 1559, ” alionya Dk. Mvungi
Aidha, ameongeza kuwa tangu GGML ianzishwe, imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na mamlaka za serikali za mitaa kusaidia miradi kadhaa ya jamii katika mkoa wa Geita kupitia Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi pamoja na programu za Kitaifa.
Dkt. Mvungi amesema, “Novemba 2022, GGML ilitambuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kama mlipakodi anayekidhi viwango vya ubora katika tasnia ya madini nchini wakati Desemba 2022, Kampuni ilinyakua tuzo mbili katika Tuzo za Chama cha Waajiri Tanzania (ATE): nafasi ya kwanza katika utekelezaji sera ya Wajibu wa Kampuni kwa jamii na mshindi wa Pili miongoni mwa waajiri bora wa sekta ya binafsi,”
Mpango huo wa mafunzo kazini, hutoa fursa kwa wahitimu wasio na ajira kupata uzoefu wa kazi ambao utakamilisha masomo yao na kuwapa uzoefu ambao unaweza kuwasaidia kukubalika katika soko la ajira na GGML inachangia katika kukuza ujuzi wa wahitimuna kuwapa fursa ya kupata uzoefu wa kazi katika nyanja mbalimbali.