Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imetoa Sh bilioni 1.6 kuunga mkono juhudi za Serikali kudhibiti maambukizi ya Virusi vya Corona ambayo hadi sasa yamesambaa katika nchi 210 duniani ikiwemo Tanzania.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na kaimu mkurugenzi mkuu wa GGML, Wayne Louw imefafanua kuwa katika fedha hizo, Sh bilioni 1.1 zitaelekezwa kwenye ngazi ya kitaifa kupitia mfuko maalum wa mapambano dhidi ya Covid – 19 ambao unasimamiwa na ofisi ya waziri mkuu.
Fedha nyingine kiasi cha Sh milioni 500 zitatumika kwa ajili ya kusaidia juhudi zinazofanywa katika ngazi ya mkoa na jamii, zitakazojumuisha ununuzi wa vifaa-tiba muhimu na vitendea kazi kama vile vifaa vya kujikinga, barakoa, mashine za kusaidia upumuaji, nk.
Aidha, GGML kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Geita (GEUWASA) imeweka matanki 10 ya maji yenye uwezo wa kubeba lita 1000 kila moja kwa ajili ya kuwezesha watu kunawa mikono.
“GGML pia itatoa dawa aina ya Chlorine ili kutakasa maji hayo, na kwa hiyo hakutakuwa na ulazima wa kutumia sabuni. Matenki mengine yanaendelea kutengenezwa kwa ajili ya watoto na watu wenye ulemavu.
“Nia yetu ni kuendelea na shughuli zetu kama zilivyopangwa na tunatumaini kwamba janga hili litakwisha hivi karibuni. Kwetu sisi, shughuli zetu zinajumuisha uzalishaji wa dhahabu na pia utekelezaji wa miradi ya kusaidia jamii inayotuzunguka,” amebainisha Louw
Naye Meneja Mwandamizi anayeshughulikia masuala ya afya mahali pa kazi, Dk. Kiva Mvungi alisema katika kujenga uelewa juu ya janga hili kwa jamii zinazozunguka mgodi, kampuni hiyo imekuwa ikigawa vipeperushi vyenye taarifa za virusi ndani na nje ya mgodi.