Kiongozi wa upinzani nchini Ghana John Mahama, amemuonya Rais wa nchi hiyo Nana Akufo-Addo, kutokufanya ‘jaribio lolote la wizi’ katika uchaguzi mkuu uliofanyika wiki hii.
Hayo yanajiri huku pande zote mbili zikidai kushinda ilihali bado matokeo rasmi yanasubiriwa, waangalizi wengi wamesema uchaguzi huo ulifanyika kwa njia ya huru na haki.
Tamko hilo la mgombea wa upinzani John Mahama, limepandisha joto la kisiasa katika nchi hiyo inayofahamika kwa utulivu licha ya kuwa katika kanda inayokumbwa na machafuko.
Mahama aliwaambia waandishi wa habari mjini Accra kwamba, baadhi ya mambo yanayofanyika hayakubaliki na kwamba Nana Akufo-Addo anaendelea kuonyesha mienendo isiyo ya kidemokrasia.
Aidha Tume ya uchaguzi inasubiriwa kutangaza matokeo rasmi, lakini ushindani mkali ulitarajiwa kati ya Mahama na Akufo-Addo.
Matokeo ya awali yanaonyesha kuwa rais Akufo-addo anaongoza kwa asilimia ndogo.