Serikali kupitia Wizara ya Afya, imejipanga kurejea upya gharama za upandikizaji wa mimba kwa wananchi wenye matatizo ya uzazi na kutopata watoto, ili kuwapunguzia mzigo wa gharama kubwa endapo watajiunga na bima ya afya kwa wote.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alipotembelea taasisi ya Kairuki iliyopo Bunju A jijini Dar es Salaam, ambayo inatoa huduma ya upandikizaji mimba kwa lengo la kuona huduma zinazotolewa kituoni hapo.
“Tatizo la kutopata watoto lipo pande zote mbili, upande wa wanaume na wanawake, lakini jamii yetu inachukulia familia isipopata mtoto basi mwanamke ndiyo anaonekana mwenye tatizo. Naamini uwepo wa kituo hiki utasaidia kuondoa fikra potofu,” amesema Waziri Ummy.
Kituo cha upandikizaji mimba cha Kairuki kinatoa huduma hiyo kwa gharama ya kuanzia Sh Mil 13 hadi Sh Mil 17 kutegemea na aina ya huduma inayohitajika ambapo Waziri Ummy pia amesema serikali itaangalia uwezekano wa kuweka nusu ya gharama katika vifurushi vya bima ya afya kwa wote, ili kuwapunguzia wananchi gharama za huduma hiyo.
“Sisi upande wa Serikali tutaendelea kuwaunga mkono na kuhakikisha kwamba huduma hizi zinatolewa na kuwafikia wengi, tumeelezwa hapa gharama za upandikizaji ni kubwa Watanzania wengi hawawezi kumudu”.
“Kwa hiyo nashukuru mmenileta kipindi hiki tunaenda kuwasilisha muswada wa bima ya afya kwa wote bungeni kwa hiyo nitaangalia uwezekano wa bima kuweza kugharamia asilimia 30 au 40 ya baadhi ya huduma zinazohitajika,” amesema Waziri Ummy.