Mlinda mlango wa AC Milan Gianluigi Donnarumma amekumbana na changamoto ya kurushiwa fedha bandia, na mashabiki wa timu ya taifa ya Italia, wakati wa mchezo wa fainali za Ulaya chini ya umri wa miaka 21 dhidi ya Denmark.
Mashabiki wa Italia wanaodhaniwa kuwa wa klabu ya AC Milan walifanya kitendo hicho kama ishara ya kumuonyesha Donnarumma, hawakupendezwa na maamuzi yake ya kugoma kusaini mkataba mpya.
Mashabiki hao wanaamini kukataa kwa mlinda mlango huyo kinda, huenda kunatokana na msukumo wa tamaa ya fedha ambazo huenda akalipwa na klabu itakayomsajili kama ataondoka 2017/18.
Donnarumma mwenye umri wa miaka 18, hakuonyesha kushtushwa na tukio hilo la mashabiki na badala yake aliendelea kuitumikia timu yake ambayo ilimaliza dakika 90 kwa ushindi wa mabao mawili dhidi ya Denmark.
Donnarumma ambaye ameshaitumikia klabu ya AC Milan kwa zaidi ya michezo 70 baada ya kupandishwa kwenye kikosi cha kwanza mwaka 2015, amekua na msimamo wa kutaka kuondoka klabuni hapo, na shinikio lake la kwanza ni kukataa kusaini mkataba mpya.
Hata hivyo mpaka sasa haijafahamika ni wapi atakapoelekea endapo AC Milan wataamua kumuweka sokoni katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi, ama kuondoka mwishoni mwa msimu wa 2017/18.
Taarifa za kugoma kwa Donnarumma, zilitolewa na mtendaji mkuu wa AC Milan Marco Fassone mwishoni mwa juma lililopita kupitia vyombo vya habari. Kiongozi huyo alikua na mazumgumzo ya kina na Donnarumma kwa majuma kadhaa, lakini mambo yalikwenda ndivyo sivyo.