Shirikisho la riadha RT, limethibitisha kukamilisha sehemu kubwa ya maandalizi ya michuano ya Afrika mashariki na kati chini ya umri wa miaka 18, ambayo yataunguruma kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es salaam kesho Jumamosi na keshokutwa Jumapili.
Katibu mkuu wa RT Wilhem Gidabudai amesema tayari baadhi ya timu shiriki zimeanza kuwasili na nyingine zipo njiani hivyo wana matarajio makubwa ya kuwa na michuano yenye ushindani.
Gidabidai amesema timu iliyotangulia kuwasili Dar es salaam ni Djibout ambayo ilifika juzi usiku kwa usafiri wa ndege.
“Djibout walikuwa wa kwanza kuthibitisha kushiriki, na wamekua wa kwanza kufika Dar es salaam, wametufurahisha sana kwa kuonyesha wanajali michuano hii mikubwa kwa vijana katikaukanda wa Afrika mashariki,”
“Zanzibar wataingia Dar es salaam leo kwa usafiri wa boti.”
“Tunatarajia kuwa na timu zenye ushindani mkubwa na kwa kanuni za shirikisho la riadha la kimataifa IAAF, zinatupa nafasi ya kuanza michuano hii kwa sababu tumevuka nusu.” Amesema Gidabudai
Timu nyingine ambayo ilitarajiwa kuwasili jana usiku ni Sudani kusini ambayo ilisafiri kwa njia ya barabara ikipitia nchini Uganda.
Timu nyingine zitakazoshiriki michuano hiyo itakayoanza rasmi kesho katika uwanja wa taifa Dar es salaam, ni wenyeji Tanzania, Uganda, Kenya, Ethiopia na Zanzibar.