Mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya ltalia, Giorgio Chiellini, ametangaza kustaafu soka, akiwa na umri wa miaka 39.
Chiellini aliyeiongoza Italia kutwaa Kombe la Euro 2020, akiwa nahodha, ametangaza kutundika daluga baada ya kucheza kwa miaka 23.
Beki huyo aliyejitengenezea jina zaidi akiwa Juventus, Juni, mwaka jana (2022), alijiunga na kikosi cha Los Angeles ya Ligi Kuu ya Marekani.
Chiellini alitoa taarifa ya kustaafu kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii huku akisisitiza kuwa, hatasahau matukio mbalimbali aliyowahi kukutanana nayo katika kipindi alipokuwa mchezaji.
“Soka ilikuwa kila kitu kwangu, hivi sasa sina budi kupumzika na kuacha mchezo nilioupenda kwa muda mrefu, kikubwa ambacho sitakisahau ni matukio mbalimbali niliyowahi kukutana nayo, sasa nakwenda kuanza maisha mapya,” aliandika.
Mchezaji huyo alianza kucheza soka mwaka 2000 katika timu ya Livorno kabla ya kujiunga na Ligi Kuu ya Italia na kuwa mmoja wa wachezaji tegemeo.
Beki huyo wa kati, alisaidia Juventus kutwaa mataji tisa ya Ligi Kuu ya Italia, kuanzia mwaka 2011 hadi mwaka 2020, ikiweno Kombe la Ligi mara tano.
Awali Chiellini, alitangaza kustaafu soka katika timu ya taifa ya Italia mwaka 2022 baada ya kucheza mechi 117 na kufunga mabao manane.