Baada ya kikosi cha Young Africans kuambulia kisago cha mabao 2-1 dhidi ya ZANACO FC, Mkurugenzi wa kampuni ya GSM inayoifadhili klabu hiyo kongwe katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, Ghalib Said Mohamed amesema ana matumaini makubwa na kikosi chao.
Ghalib ametoa kauli hiyo baada ya kuwa shuhuda kwenye mchezo huo wa kimataifa wa kirafiki uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumapili (Agosti 29), ambapo amesema kupoteza kwa ZANACO FC kutakua mwanzo mzuri kwa benchi la ufundi kufanya marekebisho kabla ya mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Rivers United ya Nigeria.
“Matokeo mabaya tuliyopata yanatujenga kuboresha upungufu ulioonekana. Ni mapema sana kukosoa usajili kwani timu ndio bado, ina nafasi ya kukaa pamoja muda mrefu ili kujiweka fiti kabla ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika,”
“Naiona Young Africans iliyo bora msimu ujao, nauona utakavyokuwa ushindani mkubwa ndani na nje kutokana na kusajili wachezaji wengi wenye uzoefu na walio na uchu wa mafanikio.” amesema Ghalib.
Hii ni mara ya kwanza kwa Ghalib kuzungumza hadharani na kunukuliwa na vyombo vya habari, jambo ambalo limekua tofauti sana, hasa ikizingatiwa mara nyingine anayezungumza kuhusu Young Africans kutoka GSM ni Injinia Hersi Said.