Uongozi wa klabu ya Simba SC umethibitisha kupokea ripoti ya Kocha Mkuu Didier Gomes, baada ya kukamilika kwa msimu wa 2020/21.
Simba SC imemaliza msimu wa 2020/21 kwa kutetea Ubingwa wa Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho, huku ikifika hatua ya Robo Fainali katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba SC, Salim Abdallah ‘Try Again’ amesema wataanza kuifanyia kazi ripoti ya Kocha Gomes kwa vitendo na watafanikisha kila hitaji aliloagiza ili kuwa na kikosi bora msimu ujao 2021/22.
“Kila kitu kinaenda vizuri, Wanasimba wanatakiwa kutulia na kusubiri waone kazi yetu inayofanywa na viongozi wao, baada ya kupokea ripoti ya Kocha Gomes Gomez Da Rosa na kufanyia kazi.”
“Mapendekezo yake makubwa ni maboresho ya kikosi kwa kufanya usajili wa wachezaji wenye kiwango kizuri na kuwa na kikosi imara ambacho ni ‘Unbeaten’.” amesema Try Again.
Licha ya kujipanga kutetea Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ta tano mfululizo na Kombe la Shirikisho kwa mara ya tatu mfululizo msimu ujao 2021/22, Simba SC pia itashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayoanza rasmi mwezi Septemba.