Kocha mkuu wa Simba SC Didier Gomed da Rosa amesema hana muda wa kujibu tuhuma alizorushiwa na wakala wa mshambuliaji kutoka nchini Rwanda Meddie Kagere.

Patrick Gakumba, wakala wa mshambuliaji huyo alimtuhumu Gomes, baada ya Meddie Kagere kushindwa kutumika wakati wa mchezo wa mkondo wa pili wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Kaizer Chiefs.

Gakumba, alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini kwao Rwanda na Tanzania, akisema kutolewa kwa Simba kwenye michuano ya Afrika kumechangiwa na kocha Gomes kwa kushindwa kumtumia Kagere.

Akizungumza na waandishi wa habari Kocha Gomes amesema: “Sitaki kuongelea kuhusu matatizo ya Patrick Gakumba, sijui chochote kuhusu malalamiko yake na siwezi kuzungumzia.”

“Sina tatizo na mshambuliaji wangu [Kagere], wiki tatu zilizopita nilizungumza na washambuliaji wote watatu [Kagere, Bocco na Mugalu] kwamba wanatakiwa kukubali na kuheshimu maamuzi yangu.”

“Kuna wakati Bocco atacheza, kuna wakati Kagere atacheza na kuna muda watacheza washambuliaji wawili. Mechi dhidi ya Mwadui Kagere alianza baadaye akaingia Bocco.”

“Sijasikia malalamiko yoyote kutoka kwa wachezaji wangu na wanafahamu kama wanataka kulalamika wanajua mlango wangu upo wazi wanaweza kuzungumza na mimi sio meneja.”

“Kila mtu anafahamu Kagere anafanya kazi nzuri, mimi sina tatizo na mtu yeyote.”

Licha ya kushinda mabao 3-0 dhidi ya Kaizer Chiefs, Simba SC ilitolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kufuatia kupoteza kwa mabao 4-0 kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa Johannesburg Afrika Kusini Mei 15.

Mabao ya Simba SC katika mchezo wa mkondo wa pili uliopigwa jijini Dar es salaam, yalipachikwa wavuni na mshambuliaji John Bocco aliyefunga mawili huku Clatous Chama akifunga bao la tatu.

Rais wa Ufaransa kufanya ziara Rwanda
Tanzania yapewa mkopo wa Bilioni 323