Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, Didier Gomes ameonesha matumaini makubwa kwa wachezaji wake wapya Sadio Kanoute, Osamane Sakho na Duncan Nyoni.
Wachezaji hao watatu ni miongoni mwa wachezaji waliosajiliwa Simba SC mwanzoni mwa msimu huu, ikiwa ni sehemu ya maboresho yaliyofanywa na Benchi la Ufundi linaloongozwa na Kocha Gomes.
Kocha huyo kutoka nchini Ufaransa amesema Kanoute, Sakho na Nyoni wanaendelea kuzoea mazingira ya Tanzania, na muda si mrefu wataanza kuonyesha makali yao na kikosini.
“Sadio Kanoute, Sakho na Nyoni wanakuja vizuri na naamini watakuja kuleta vitu vizuri siku za mbele. Najiamini sana kutakuwa na mambo mazuri siku za mbele, wachezaji wote wanabadilika kiuchezaji.”
“Tumeanza kubadilika eneo la ushambuliaji. Kiukweli kuondoka kwa Luis na Chama unatakiwa utafute njia nyingine ya kwenye ushambuliaji. Tupo njia sahihi mpaka sasa,” amesema Kocha Gomes
Kocha Gomes jana alianza rasmi maandalizi ya kikosi chake kuelekea mchezo wa Mkondo wa Pili wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya Kwanza dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana, utakaochezwa Jumapili (Oktoba 24) Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.