Benchi la Ufundi la Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, limeanza kazi ya kuisoma Jwaneng Galaxy kupitia picha za Video, kwa kuwashirikisha wachezaji.
Simba SC, itaanzia ugenini katika mchezo wa Mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana Oktoba 17, kabla ya kucheza mchezo wa Mkondo wa pili jijini Dar es salaam Oktoba 22.
Kocha Mkuu Didier Gomes akisaidiwa na Thierry Hitimana na Seleman Matola, tayari amepata baadhi ya majina ya nyota wa Jwaneng Galaxy ambao ni Bertrand ambaye ni usajili mpya kutoka Rwanda katika klabu ya Gasoline United na Gape Mohutsiwa.
Kocha Msaidizi wa Simba, Hitimana amesema wameanza kuwafuatilia wapinzani wao licha ya kuangalia michezo ya nyuma kuanzia Februari 2021, ambapo walikuwa kwenye ligi na michuano hiyo ya hatua za awali.
Amesema hatua hiyo ni baada ya kuchelewa kuanza kwa Ligi Kuu ya Botswana hali iliyopelekea kukosa mechi nyingi za wapinzani hao.
“Tumeanza kuwafuatilia licha ya wenzetu ligi yao imechelewa kuanza, tunatumia mechi za hivi karibuni pamoja na taarifa za wachezaji wao ikiwemo usajili waliofanya kwa mchezaji kutoka Rwanda,” amesema Kocha huyo.
Amesema wanatambua umuhimu wa mechi hiyo pamoja na ushindani wao na kuhakikisha kutumia vizuri ya kalenda ya FIFA na wachezaji waliobaki kufanya maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Jwaneng Galaxy.
“Hawa waliobaki katika timu tutaanza nao mazoezi mepesi, kisha baada ya hapo tutakwenda kwenye mbinu ambayo na wale waliokuwa timu za taifa wataungana na wenzao katika hili,” amesema.
“Baada ya hapo tutakuwa na muda mwingi wa awamu ya kuangalia mechi za Galaxy – zile za mashindano ya kwao na mchezo wa hatua ya kwanza waliocheza kisha kufahamu ubora na upungufu waliokuwa nayo,” amesema kocha huyo.
Amesema kutokana na mipango waliyonayo kwa wachezaji na mbinu wanazofanya kipindi hiki, wana matarajio makubwa ya kwenda kufanya vizuri katika michezo yote miwili ya ugenini na nyumbani dhidi ya Watswana hao na kufuzu kucheza makundi.