Licha ya kuwa na uhakika wa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara Msimu huu 2020/21, Kocha Mkuu wa Simba SC Didier Gomes amesema mpango huo hautokua rahisi kama Mashabiki na Wanachama wanavyofikiria.

Simba SC inahitaji alama tatu tu! kutimiza lengo la kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara kwa mara ya nne mfululizo, lakini jukumu zito lililo mbele yao ni kuhakikisha wanaifunga Young Africans, kwenye mchezo ujao wa Ligi Kuu, utakaochezwa Julai 03 Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes amesema mchezo ujao wa Ligi Kuu dhidi ya watani wa jadi Young Africans utakuwa mgumu, ingawa anaimani kuwa, kikosi chake kitapambana kwa lengo la kuhitaji alama tatu muhimu.

“Tumebakisha michezo mitano na tunahitaji alama tatu tu! tutangazwe mabingwa na mchezo unaofuata ni dhidi ya watani zetu Young Africans, najua itakuwa kama fainali, nawaamini wachezaji wangu na tutafanya vizuri na kuibuka washindi,” amesema Gomes.

Baada ya kuifunga Mbeya City FC mabao 4-1, juzi Jumanne (Juni 22) Simba SC imefikisha alama 73 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiiacha Young Africans yenye alama 67 zinazoiweka nafasi ya pili huku Azam FC wakiwa nafasi ya nne kwa kumiliki alama 64.

Kwa sasa Simba SC inajiandaa na mchezo wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC), utakaochezwa mjini Songea mkoani Ruvuma dhidi ya Azam FC, Jumamosi (Juni 26), Uwanja wa Majimaji.

Mchezo mwingine wa Nusu Fainali ya michuano hiyo utachezwa kesho Ijumaa (Juni 25) mjini Tabora kati ya Young Africans dhidi ya Biashara United Mara, Uwanja wa Alli Hassan Mwinyi.

Gomes afichua siri ya kumchezesha Chama
Mhariri Mtendaji wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo afariki dunia