Kocha Mkuu wa Simba SC Didier Gomes amesema anafikiria kuwapumzisha baadhi ya wachezaji wake, baada ya kufanikiwa kutetea Ubingwa wa Tanzania Bara kwa mara ya nne mfululizo.
Kocha Gomes ametangaza mpango huo alipozungumza na waandishi wa habari, baada ya kikosi chake kuibanjua KMC FC mabao 2-0, yaliofungwa na Mshambuliaji wao kutoka DR Congo Criss Mutshimba Koppe Mugalu dakika ya 3 na 44.
Gomes amesema: “Tumefanikiwa kutetea ubingwa, nafikiri kuwapumzisha baadhi ya wachezaji ambao wametumika zaidi na kuwapa nafasi wengine.”
“Ligi ilikuwa ndefu na mechi zilikuwa karibu karibu na pia tunajiandaa na fainali ya FA.”
“Simba ni familia kuna wachezaji wananivutia sana mazoezini lakini kutokana na ukubwa wa kikosi wamekosa nafasi, Miraji Athumani, Said Ndemla ni miongoni mwao wanafanya vizuri na nafurahi kufanya nao kazi,”
Ushindi dhidi ya KMC FC unaifanya Simba SC kufikisha alama 76 ambazo zinaweza kufikiwa na Young Africans pekee, endapo itashinda michezo yake miwili iliosalia.