Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, Didier Gomes amesema bado ana deni kubwa ndani ya klabu hiyo, licha ya kuacha alama kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Kocha Gomes ametoa kauli hiyo baada ya kikosi chake kutupwa nje ya michuano hiyo mikubwa barani Afrika upande wa vilabu, ambapo amesema mipango na mikakati yake ni kuivusha Simba SC kwenye hatua ya robo fainali ili icheze nusu fainali au fainali.

Amesema ilikua kama bahati mbaya kwa kikosi chake kushinda kufuzu kucheza nusu fainali kwa msimu huu, lakini amewataka mashabiki na wanachama kuendelea kushikamana na timu yao ili imrahisishie kufikia lengo msimu ujao.

“Bado nina deni ambalo natakiwa kulilipa Simba pamoja na kuweka alama kwenye mashindano haya (CAF) kwa kufika hatua hii tuliyofika kwa mara ya pili mfululizo.”

Kuhusu mapambano ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2020/21, Kocha huyo kutoka nchini Ufaransa amesema ni muda muafaka kwake kutimiza lengo la kutetea ubingwa wa VPL kwa mara ya nne mfululizo.

Amesema mbali na kutetea ubingwa wa VPL, pia amejipanga kupambania ubingwa wa Kombe la Shirikisho ambapo siku ya Alhamis watacheza dhidi ya Dodoma Jiji FC, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

“Sasa nguvu zetu tunakwenda kuziweka katika mashindano ya ndani na kuchukua kila kombe lililopo mbele yetu kutokana na ubora wa kikosi kilivyo naona tuna kila sababu ya kufanya hivyo.”

Simba SC ilishindwa kusonge mbele kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, licha ya kuchomoza na ushindi wa mabao matatu kwa sifuri dhidi ya Kaizer Chiefs, Jumamosi Mei 22, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Mabao manne kwa sifuri waliyofungwa wawakilishi hao wa Tanzania kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa Afrika kusini Mei 15, ndio yamewasukuma nje ya michuano hiyo Simba SC.

Serikali iwaachie wawekezaji ama wananchi - Ndugai
Yacouba Sogne awakuna viongozi Young Africans