Kuelekea Mchezo wa Fainali Kombe la Shirikisho (ASFC), kati ya mabingwa watetezi Simba SC dhidi ya Young Africans, waamuzi watakaopangwa kuchezesha mchezo huo wameombwa kuwa makini wakati wote.

Ombi hilo kwa waamuzi linetolewa na Kocha Mkuu wa Simba SC Didier Gomes jijini Dar es salaam, alipokua akizungumza na waandishi wa habari.

Kocha huyo kutoka nchini Ufaransa amesema mchezo wa Fainali ni mchezo muhimu na unapaswa kuchezeshwa na waamuzi wenye ufanisi wa hali ya juu.

Amesema haitapendeza kuacha maswali mengi kwa mashabiki baada ya mchezo wa Fainali, kama ilivyokuwa Jumamosi ya Julai 03 walipocheza dhidi ya Young Africans.

Amesema mchezo katika huo, timu yake haikutendewa haki, kufuatia kunyimwa penati mbili za wazi na Mwamuzi Emmenuel Mwandembwa.

“Mwamuzi alitunyima penati mbili za wazi kwenye mchezo dhidi ya Yanga, sasa hilo sio jambo zuri, huo ni mchezo wa fainali mwamuzi lazima awe makini na kuona matukio yote kwa usahihi ili mshindi apatikane kihalali” amesema Gomes

Mchezo wa Fainali Kombe la Shirikisho (ASFC) utachezwa Julai 25 mkoani Kigoma, Uwanja wa Lake Tanganyika.

Kisu kinavyotumika kufanya “masaji” ya mwili
Marekani yakataa kutoa msaada wa kijeshi kwa Haiti