Imeripotiwa kuwa Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, Didier Gomes amelazimika kubadili mfumo wake katika kikosi chake ili kutoa nafasi kwa majembe mapya yaliyoingia kikosini ambao yameonekana kumpasua kichwa jinsi ya kuwatumia.
Awali Gomes alikuwa akitumia mfumo wa 4-2-3-1, 4-3-3 au 4-4-2 (D), lakini kwa sasa ameutambulisha mfumo mpya wa 3-5-2 uliokuwa awali ukitumiwa na mtangulizi wake, Svena Vanderbroeck aliyetimkia FAR Rabat ya Morocco mwishoni mwa mwaka 2020.
Mfumo huo unatumia mabeki asilia wa kati watatu, viungo watano ambao asilia wanakuwa watatu pamoja na mabeki wa pembeni wawili wanaunda eneo la kiungo kisha washambuliaji asilia wanakuwa wawili.
Kwa sasa ameamua kuutumia mfumo huo kutokana na ubora ambao wamekuwa wakionyesha mabeki wa kati, Hennock Inonga, Joash Onyango, Pascal Wawa, Erasto Nyoni na Kennedy Juma.