Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Didier Gomes amesisitiza ushindi kuelekea mchezo wa kesho wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya Makundi dhidi ya Al Merrikh, utakaochezwa kesho Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es salaam.

Kocha Gomez amesisitiza jambo hilo, alipozungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo mchana jijini Dar es salaam, ikiwa ni sehemu ya kukamilisha maandalizi ya kuelekea mchezo huo utakaoanza majira ya saa kumi jioni.

Amesema kuna ulazima wa kikosi chake kupambana na kusaka ushindi kwenye mchezo huo, ambao anaamini utakua na ushindani wa hali ya juu, lakini akasisitiza kuwa Simba ina faida ya kucheza nyumbani na kuitumia nafasi hiyo ili kufikia lengo la kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

“Lazima tushinde, ni muhimu sana kupata alama tatu kesho sababu kwenye hili kundi ili kufika robo fainali tunahitaji alama 11 hivyo ni muhimu sana kushinda. Kwa nilichokiona kwenye mazoezi kwa siku hizi tupo vizuri.” Amesema Kocha Didier Gomes.

Naye nahodha wa kikosi cha Simba SC John Bocco amesema: “Tupo nyumbani na tupo tayari kupambana kwa ajili ya timu na kupata alama tatu. Tunashukuru kwa ushirikiano tunaopata kwa mashabiki ingawa tunajua kwamba kesho hawatakuwepo uwanjani lakini tunaamini kwa dua zao tutapata ushindi.”

Simba SC inaendelea kuongoza msimamo wa kundi hilo kwa kufikisha alama 07, baada ya kuzifunga AS Vita na Al Ahly, huku akitoka sare ya bila kufungana dhidi ya Al Merrikh.

Azam FC kutumia udhaifu wa Young Africans
Lwanga kuikabli Al Merrikh kesho