Kocha wa Tabora United, Goran Kopunovic amesema endapo ataingia kwenye usajili wa dirisha dogo, basi atatafuta washambuliaji wenye makali ya kufunga mabao na pamoja mabeki.
Kopunovic amesema mipango yake ya muda mfupi ni kuendelea kuwaongezea makali washambuliaji alionao sasa kwenye kikosi hicho cha Ligi Kuu Tanzania Bara, huku ile ya muda mrefu ni kuanza kutafuta washambuliaji na mabeki walio bora.
Kwenye mechi tisa ilizocheza Tabora imejikuta ikipata suluhu kwenye mechi tano dhidi ya Singida Big Stars, Coastal Union, KMC na Kagera Sugar.
Timu hiyo imeshinda mechi mbili dhidi ya Tanzania Prisons na Dodoma Jiji huku wakipoteza mbili mbele ya Azam FC na JKT Tanzania ilkiwa kwenye nafasi ya saba katika msimamo wa Ligi Kuu Bara.
“Tunakabiliwa na changamoto ya kufunga mabao. Tumefanikiwa kufunga, lakini sio kwa kiwango ambacho kinatakiwa kulingana na nafasi ambazo tunatengeneza,”amesema Kopunovic.
“Tutaendelea kulifanyia kazi lakini muda ukifika tutaangalia namna nzuri ya kuleta watu bora zaidi ambao watakuja kutuongezea upande wa kiungo mkabaji, kiungo mshambuliaji na beki wa kulia ili tuwe na nguvu.”
Katika mechi hizo tisa, Tabora United imefanikiwa kufunga mabao matano huku ikiruhusu mabao saba ikiwa ndio msimu wake wa kwanza kwenye ligi tangu ipande msimu huu.
“Kuna maboresho tutalazimika kuyafanya tutahitaji watu wa kuja kutuongezea nguvu wenye ubora, nafurahia kazi inayoendelea kuonyeshwa na vijana tulionao, wanafanya kazi kubwa lakini tutahitaji ziadi kwa siku za karibuni,” amesema kocha huyo wa zamani wa Simba SC.