Kocha Mkuu wa Tabora United, Goran Kopunovic amewataka wachezaji wa timu hiyo kuongeza umakini zaidi kwa michezo ya ugenini na kuacha mazoea ya kuonyesha soka safi wakati ikiwa kwenye uwanja wake wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora.

Kauli ya Goran inajiri baada ya timu hiyo kuchezea kichapo cha bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi juzi Jumatano (Oktoba 25), na kuifanya kupoteza mechi ya pili msimu huu baada ya Agosti 16, mwaka huu kufungwa pia na Azam mabao 4-0.

“Tunahitaji kuonyesha kiwango kizuri katika kila mchezo kwa sababu kwa mwenendo huu sio mzuri kwetu na hatuwezi kufikia malengo tuliyojiwekea, nawapongeza wachezaji kwa jitihada zao lakini hatupaswi kuishia tu hapa tulipo sasa,” amesema.

Goran ameongeza sababu kubwa iliyowaangusha katika mchezo huo ni kukosa umakini kwa wachezaji kuanzia eneo la ulinzi hadi ushambuliaji jambo ambalo kwake ni changamoto anayoenda kuifanyika kazi kwenye uwanja wa mazoezi ili lisijirudie.

Katika michezo saba wameshinda miwili, sare mitatu na kupoteza miwili ikiwa nafasi ya saba na pointi tisa.

“Tuna siku kadhaa za kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza kabla ya kucheza na Kagera Sugar Oktoba 30, ni mchezo mwingine mgumu kutokana na matokeo pia ya wapinzani wetu waliyoyapata ila tutapambana.”

Umaarufu wa ANC wazidi kuporomoka
Wizara, JICA wajipanga usambazaji Gesi asilia