Serikali itaanza kuzitazama ajira za vyuo vikuu ambapo badala ya kuangalia ubora wa ufaulu (GPA) pekee, sasa itaajiri kwa kupimwa uwezo wa mtu kwa kufanya usaili kwani GPA pekee haitoshi.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda mbele ya Mgeni rasmi Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philiph Mpango katika mahafali ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyofanyika Jijini Dar es Salam.
Amesema, “Kuangalia ufaulu pekee wa Wanafunzi haitoshi kuboresha elimu badala yake ni muhimu kuongeza vigezo hivyo katika mapitio ya sera na mabadiliko ya mitaala, hilo litatazamwa kwa weledi mkubwa.”
Aidha ameongeza kuwa, wakati Serikali ikiongeza udahili wa Wanafunzi haitokuwa tayari kuona ubora unapungua hivyo inaendelea na mkakati wake wa kuhakikisha ubora wa elimu hususani katika Vyuo Vikuu unaimarika.