Meneja wa Klabu ya Chelsea Graham Potter, amewatoa hofu Mashabiki wa Klabu hiyo kwa kusema Beki wa Pembeni Reece James yupo sawa na hana jeraha kubwa kama ilivyofikiriwa.
James alilazimika kutolewa dakika ya 53 wakati wa mchezo wa Ligi Kuu ya England dhidi ya FC Bournemouth iliyokubali kupoteza kwa mabao 2-0, jana Jumanne (Desemba 27).
Beki huyo alitolewa kufuatia jeraha la Goti, ambalo wengi walihisi huenda lingekuwa kubwa na kupelekea kukosa baadhi ya Michezo ya Klabu ya Chelsea iliyosalia hadi mwishoni mwa msimu huu.
James mwenye umri wa miaka 23, alikua anarejea Uwanjani kwa mara ya kwanza baada ya kupona jeraha la Goti, ambalo lilimlazimu kuondolewa kwenye Kikosi cha England kilichoshiriki Fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar.
“Ni aneo lile lile ambalo aliumia mwanzo, lakini imethibitika sio jeraha kubwa sana,”
“Ni mapema mno kwake kuumia tena katika eneo ambalo aliliuguza kwa zaidi ya mwezi moja uliopita, inasikitisha sana kama binaadamu, lakini nimethibitishiwa atakua vizuri na atarejea Uwanjani kupambana na wenzake kwa ajili ya Chelsea”
“Huenda ikachukua muda wa saa 24 hadi 48 atakuwa vizuri na kurejea kwenye mazoezi ya kikosi. Najua Mashabiki walishtushwa na kilichotokea hasa nilipoamua kumtoa nje, lakini niwatowe wasiwasi James yupo salama.”
“Alivunjika Moyo sana kuzikosa Fainali za Kombe la Dunia, ilikua ni moja ya Ndoto zake kubwa kucheza Fainali za Qatar, Hata hivyo amethibitisha kuwa yupo vizuri na ndio maana leo amecheza katika kiwango kikubwa kabla ya kupata maumivu.” amesema Potter
Mabao ya Chelsea kwenye mchezo dhidi ya FC Bournemouth yalikwamishwa wavuni na Kai Havertz na Mason Mount katika dakika ya 16 na 24.