Kozi ya makocha wa mpango wa Grass Roots unaolenga wachezaji mpira wa miguu (wasichana na wavulana) wenye umri kati ya miaka 6-12, imefanyika kwa mafanikio mkoani Lindi.

Kozi hiyo ilifungwa rasmi  Jumapili Novemba 19, 2017 na Mkuu wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga katika hafla iliyofanyika Uwanja wa Ilulu mkoani Lindi.

Akifunga kozi hiyo iliyoshirikisha walimu  30 wa shule za msingi  kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Lindi  kwenye Uwanja wa Ilulu Lindi,  Mkuu wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga amewakumbusha kuwa elimu waliyoipata waitumie kama chachu ya kukuza soka la Tanzania,

“Mkoa wa Lindi umepata bahati kubwa sana kupata elimu hii kwani awali tulijua ni kwa ajili ya Mkoa wa Dar ila kumbe hata sisi huku Lindi Vijijini tunatambuliwa na TFF, Nitatoa ushirikiano kwa waalimu wote 30 waliopata mafunzo ili tuweze kukuza soka letu hasa Wilaya yetu ya Lindi,” amesema.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi amewapongeza washiriki wote waliopata kozi hiyo huku akiwahasa kutumia elimu waliyoipata kufundishia michezo mashuleni.

“Waalimu sina shaka na nyie, nyie ni bado vijana natambua elimu mliyoipata itaufanya mkoa wa lindi kupata vijana wengi wakiume na wakike ambao watapata elimu ya soka kutoka kwenu, ikumbukwe dhumuni la TFF ni kutoa elimu kwenu ili nyie mkaitumie kwa vijana mashuleni,” amesema.

Madadi amewataka washiriki kuitumia vizuri nafasi hiyo waliyoipata kwa kwenda kuwafundisha na kuupenda mpira wa miguu watoto wadogo wenye umri kati ya miaka 6-12.

Ikumbukwe kozi hii ya Grass Roots kwa mwaka huu imefanyika mara mbili ambapo mwezi Septemba na  Oktoba  zilifanyika Dar kwenye Ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania kwa kushirikisha waalimu wa shule za msingi na Sekondari kutoka mkoa wa Dar es saalam.

Mnangagwa amkomalia Rais Mugabe ajiuzulu
JPM awafunda Msando na Masha