Kiungo Mshambuliaji, Mason Greenwood amewekewa mezani dili la Pauni 10 milioni kwenda kukipiga Saudi Arabia huku ikielezwa kwamba kocha wake wa zamani Jose Mourinho naye anamtaka akacheze kwenye kikosi cha AS Roma, Italia.

Siku moja tu baada ya Manchester United kutangaza kuachana na Greenwood, klabu ya Al-Ettifaq ya Saudi Arabia inayonolewa na Steven Gerrard inapiga hesabu za kwenda kunasa saini yake ili akajiunge na timu yao.

Kuna klabu nyingine za Saudia zinahitaji pia huduma ya mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 21.

Hata hivyo, Greenwood hayupo tu kwenye rada za AS Roma ya Italia inayonolewa na Mourinho, aliyemnoa mchezaji huyo walipokuwa pamoja Man United, bali pia mshambuliaji huyo anasakwa na Galatasaray ya Uturuki.

Al-Ettifaq inaripotiwa kuongoza kwenye mbio za kumfukuzia Greenwood ikimtengea dili la mshahara wa Pauni 10 milioni kwa mwaka.

Timu hiyo ndiyo anayochezea nahodha msaidizi wa England, Jordan Henderson, aliyenaswa kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi akitokea Liverpool na kulipwa mshahara Pauni 700,000 kwa juma.

Kuhusu Galatasaray wao walimchukua Wilfried Zaha bure kutoka Crystal Palace na walimsajili winga Hakim Ziyech kwa mkopo kutoka Chelsea.

Taarifa zinafichua: “Jose alimpigia simu baba yake Mason na alizungumza na Mason mwenyewe pia.

Alimwambia njia bora ya kupambana na hali inayomkabili ni kucheza soka. Mason alivutiwa sana na jambo hilo na kuhamasika.”

Kuna timu kibao zinamtaka Greenwood ikiwamo Juventus, AC Milan na Inter Milan zote za Italia.

Greenwood amefunga mabao 35 katika mechi l29 alizochezea Man United.

TFF, Bodi ya Ligi zakosolewa
Mwakinyo kuzichapa na Mkenya