Meneja wa FC Barcelona Ronald Koeman amesema mshambuliaji kutoka nchini Ufaransa Antoine Griezmann atakua sehemu ya wachezaji watakaokua chaguo lake la kwanza kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu ya Hispania (La Liga).

Ujio wa meneja huyo kutoka nchini Uholanzi, umekua chungu kwa baadhi ya wachezaji waliokua wamezoeleka klabuni hapo, na tayari mshambuliaji Luis Suarez ameshapewa ruhusa ya kuondoka, huku nahodha Lionel Messi akiendelea kuhusishwa na harakati za kuikacha Barcelona na kutimkia England.

Suarez anaendelea na mpango wa kuihama klabu hiyo ya Cataluña, na mabingwa wa soka nchini Italia Juventus FC wamehusisha na harakati za kumsajili, huku Atletico Madrid wakiazimia kumbakisha Hispania.

“Kwa heshima zote, Griezmann lazima arejee kucheza katika nafasi aliyozoea kutoka kwa waajiri wake wa zamani na timu ya taifa. Hapa ndipo msaada na ushauri wa kocha unahitajika zaidi,” amesema Koeman.

Kwa mujibu wa wakala Eric Olhats, Griezmann alikuwa tayari kuondoka Camp Nou mwishoni mwa msimu huu baada ya kulazimika kucheza katika nafasi ambayo hajaizoea kila mara alipowajibishwa kwa pamoja na Messi na Suarez katika klabu ya Barcelona.

“Alishiriki kikao na Koeman ambaye kwa sasa amemhakikishia kwamba atamchezesha katika nafasi inayomfaa zaidi uwanjani,” akasema Olhats.

Griezmann ambaye ni mzawa wa Ufaransa, alisajiliwa FC Barcelona kutoka Atletico Madrid kwa ada ya uhamisho ya shilingi za kitanzania bilioni 14 mwanzoni mwa msimu wa 2019-20.

Hata hivyo, hakuridhisha jinsi ilivyotarajiwa huku akichezeshwa kwa dakika zote 90 katika mchezo mmoja, miongoni mwa michezo aliocheza msimu uliopita.

Chini ya mameneja Ernesto Valverde na Quique Setien waliotimuliwa klabuni hapo msimu huu, Griezmann alifunga mabao 15 pekee kutokana na michezo 48.

“Alikuwa amefikia maamuzi ya kuagana na Barcelona hata kabla ya mchezo wa Robo-Fainali ya UEFA iliyowashuhudia wakipigwa mabao manane kwa mawili dhidi ya mabingwa wa Ulaya FC Bayern Munich.”

“Dalili zote ziliashiria kwamba hakuwa sehemu ya mipango ya klabu, na hakuwa katika mawazo ya kocha. Hata hivyo, kwa sasa yuko radhi kusalia Camp Nou na Koeman atamuunga mkono kwa mengi,” aliongeza Olhats.

Kwa mujibu wa gazeti la L’Equipe, Griezmann kwa sasa atavaa jezi namba saba mgongoni badala ya 17 msimu ujao.

Kigoma : 146 mbaroni kwa ujambazi, mauaji
Tutaboresha sera na mifumo, sekta ya Madini -JPM