Mkurugenzi wa Uwekezaji kampuni inayoifadhali Young Africans ‘GSM’ Mhandisi Hersi Said, amempongeza Mshauri wa klabu hiyo Senzo Mazingiza Mbatha kwa kubuni wazo na kuandaa Wananchi Medi Day tukio ambalo lilifanyika jana Jumanne (Februari 02) katika viunga vya Avic Town, Kigamboni jijini Dar es salaam
Young Africans imeandika historia nchini Tanzania kwa kuandaa tukio hilo ambalo liliwakutanisha waandishi wa habari, wadhamini, viongozi na wachezaji wa klabu hiyo kongwe katika ukanda wa Afrika Mashariki katika eneo la Avic Town, ambako kuna kambi ya kikosi chao.
Akizungumza kwa niaba ya ‘GSM’, Hersi amesema tukio hilo ni la kipekee na kwa hakika limewapa fursa wanahabari na wadau wa soka kuonana ana kwa ana na wanafamilia wa klabu ya Young Africans na kupata nafasi ya kubadilishana mawazo.
Aidha Hersi amesema ‘GSM’ itaendelea kuisapoti na kuipambania klabu ya Young Africans kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa, kuanzia msimu huu wa 2020/21, huku shabaha kubwa ikiwa ni kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara na kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao.
“Nampongeza Bwana Senzo Mbatha kwa kuanzisha tukio hili la Wananchi Media Day, pia tunafurahishwa na tunaridhishwa na namna timu inavyoendeshwa, namna uongozi wa klabu ya Young Africans unavyofanya kazi”
“Tunawaomba mashabiki na wapenzi wa Klabu ya Young Africans kuendelea kuisapoti klabu, sisi ‘GSM’ tutaendelea kuisapoti na kuipambania klabu kwa asilimia Mia Moja, kama kushinda tutashinda pamoja na kama kupoteza tutapoteza pamoja,” alisema
Nao wadhamini wakuu wa klabu ya Young Africans, kampuni ya Sportpesa wameeleza kufurahishwa na tukio hilo wakieleza kuwa ni tukio la kihistoria kufanyika kwa mara ya kwanza katika ardhi ya Tanzania
“Tumefurahishwa na klabu ya Young Africans kwa tukio waliloliandaa la Wananchi Media Day, ni tukio la kihistoria katika soka la Tanzania na klabu hii inakuwa muanzilishi wa tukio hili zuri na la kihistoria la kuwakutanisha Waandishi wa habari kuja kutembelea Training Camp ya Klabu,” alisema Mwakilishi wa Sportpesa Tanzania.