FC Barcelona wameonesha kuwa tayari kumuachia kiungo wao kutoka nchini Uturuki Arda Turan, kwa kuitaka klabu ya  Guangzhou Evergrande ya nchini China kutoa kiasi cha pauni milioni 44 kama ada ya uhamisho.

Turan amekua katika tetesi za kutaka kuihama FC Barcelona kwa kipindi kirefu kutokana na changamoto za kushindwa kucheza katika kikosi cha kwanza, tangu aliposajiliwa huko Camp Nou mwaka 2015 akitokea Atletico Madrid kwa ada ya uhamisho wa Pauni milioni 24.

Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na Spanish publication Sport, magwiji hao wa soka mjini Barcelona wamepanga kiasi hicho cha pesa kwa kuamini ipo haja ya kuingiza faida kutokana na mkataba uliopo kati yao na kiungo huyo mwenye umri wa miaka 29.

Wakala wa Turan (Ahmet Bulut) juma lililopita alikutana na viongozi wa FC Barcelona kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya kuwezesha uhamisho wa mchezaji wake.

Wakati FC Barcelona wakiweka wazi kiasi ambacho wanakihitaji kwa ajili ya uhamisho wa Turan, uongozi wa Guangzhou Evergrande umetenga kiasi cha Pauni 330,000 kama mshahara wa kila juma kwa ajili ya mchezaji huyo wa zamani wa Galatasaray.

Kiasi hicho cha pesa ni ni mara tatu ya mshahara wa Turan anaoupokea kwa sasa akiwa na FC Barcelona.

Mkakati wa usajili wa Arda Turan ni sehemu ya mipango ya klabu za soka nchini China kuendelea kuvuna wachezaji nyota kutoka barani Ulaya na kwingineko, na mpaka sasa zimeshafanikiwa kuwanasa baadhi ya wachezaji kama John Obi Mikel, Graziano Pelle, Carlos Tevez, Alex Teixeira pamoja na Hulk.

Ben Davies Atafuta Pakutokea
Diego Costa Atega Bomu Lingine Darajani