Kocha Mkuu wa Manchester City, Pep Guardiola amekataa kuzungumzia ugomvi uliotokea baada ya mchezo wa Ligi Kuu ya England baina ya timu yake na Arsenal uliowahusisha beki Kyle Walker na Kocha wa Washika Bunduki hao, Nicolas Jover, Jumapili (Oktoba 08).
Kwenye mchezo huo Uwanja wa Emirate, Arsenal waliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Brazil, Gabriel Martineli dakika ya 86 kufuatia mpira aliopiga na kumgonga beki Nathan Ake.
Lakini huku City ikishuka mpaka nafasi ya tatu kutokana na kipigo hicho na cha juma lililopita cha mabao 2-1 kutoka kwa Wolves, kulizuka mzozo wakati wa kuelekea vyumba vya kubadilishia nguo kati ya Walker na Jover ambaye amewahi kufanya kazi na Manchester City.
Jover alionekana kunyoosha mkono wake kwa Walker uliokuwa na lengo la kumsalimia lakini beki huyo wa kimataifa wa England alikataa na kumshambulia Jover.
Akizungumza baada ya mechi hiyo, Guardiola alisema hataki kuzungumzia tukio hilo ingawa alikiri kufahamu kilichotokea.
“Najua kilichotokea lakini sitaki kusema chochote. Wao Arsenal wanajua.” alisema Guardiola.
Kipigo hicho cha Man City kimetia doa matumaini ya klabu hiyo ya kuwa timu ya kwanza kwenye historia kushinda mara nne mfululizo ubingwa wa Ligi Kuu ya England.
Na Guardiola alisema kipigo hicho cha mapema kinaweza kupunguza presha kwa wachezaji wake katika suala hilo.
“Hakuna timu iliyowahi kushinda ubingwa wa Ligi Kuu ya England mara nne mfululizo,” amesema Guardiola.
“Mnaweza kufungwa, lakini ndio kwanza Oktoba. Wakati fulani ni vizuri kuwa nyuma. Msimu uliopita tulikuwa nyuma sana lakini msimu ni mrefu.
Hongera kwa Arsenal. Tunajua nini hasa tunachotakiwa kufanya na tutafanya hivyo. Tutapata unafuu, watu wanarejea kutoka majeraha na tutajaribu kufuta matokeo mabaya haraka iwezekanavyo tutakavyokutana na mechi ngumu dhidi ya Brighton. Na Wolves ilikuwa mechi ngumu.”