Meneja wa Manchester City Pep Guardiola, amemkingia kifua mkuu wa benchi la ufundi la Arsenal Mikael Arteta, ambaye kwa sasa ana wakati mgumu wa kusaka matokeo kwenye michezo ya Ligi Kuu England (EPL).

Arsenal imekua haifanyi vizuri kwenye michezo ya Ligi Kuu ya England, hali iliyopelekea kushika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi hiyo, lakini upande wa michuano ya Europa League imeshinda michezo yote ya hatua ya makundi na kusonga mbele kwenye hatua ya 32 bora.

Guardiola ambaye aliwahi kufanya kazi na Arteta kama msaidizi wake Manchester City, amesema kuna haja kwa mashabiki wa soka hususan wale wa Arsenal kumpa muda Mspaniola huyo.

“Arteta anahitaji muda ndani ya Arsenal kwa sasa kwa sababu ninamjua ni kocha mzuri na ana uwezo mkubwa wa kufundisha timu na ikapata matokeo licha ya sasa kuwa kwenye mwendo mbovu.”

“Arsenal haitapata mwalimu mzuri na mwenye uwezo wa kuifundisha timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao kwa kuwa aliyepo sasa ameanza kutengeneza misingi ya timu hiyo hivyo kwangu ninaona ni mwalimu bora.”

“Siwezi nikasema kwamba ninampa sapoti ili abaki, ila ukweli ni kwamba yeye mwenyewe anajua kila kitu na anauwezo wa kuwa bora zaidi ya hapo alipo. Anapenda kile anachokifanya namna anavyojitoa pamoja na kutimiza majukumu ndani ya timu yake kwa sasa.” Amesema Guardiola.

Akiwa kama meneja msaidizi Manchester City, Arteta aliweza kushinda mara mbili taji la Ligi Kuu England na taji la chama cha soka England (FA Cup), akiwa ndani ya kikosi cha Manchester City ambapo alikuwa ni kocha msaidizi.

Arteta alisaini mkataba wa kukinoa kikosi cha Arsenal Desemba 2019, na kufanikiwa kutwaa ubingwa wa kombe la chama cha soka nchini Engand (FA Cup) na Ngao ya Jamii.

Stephen Sey amvutia Lwandamina
Somalia yavunja uhusiano wa kidiplomasia na Kenya