Nahodha wa timu ya taifa ya Peru José Paolo Guerrero Gonzales, rasmi atazikosa fainali za kombe la dunia zitakazoanza nchini Urusi Juni 14.
Guerrero, atakua shuhuda wakati wa fainali hizo, baada ya kuthibitika anatumia dawa za kusisimua misuli, hali ambayo ilimfanya afungiwe kucheza soka kwa kipindi cha miezi sita mwishoni mwa mwaka 2017.
Hata hivyo mshambuliaji huyo anaeitumikia klabu ya Flamengo ya nchini Brazil, alipinga adhabu hiyo na kukata rufaa katika mahakama ya usuluhushi ya Michezo (CAS), lakini bado imethibitika alikua akitumia dawa hizo.
Mahakama ya CAS imetoa taarifa ya hukumu kwa Guerrero muda mchache uliopita na kumuongezea kifungo kutoka miezi sita hadi 14.
Kwa mantiki hiyo Guerrero anatarajiwa kurejea tea uwanjani mwezi Februari mwaka 2019.
Mpaka anaingia kifungoni mwezi Disemba mwaka jana, Guerrero alikua ameshaitumikia timu ya taifa ya Peru katika michezo 86 na kufunga mabao 32.