Mkutano wa kimataifa wa maendeleo ya mawasiliano umeanza rasmi jijini Kigali nchini Rwanda, ukiwa na lengo la kupitisha mwongozo wa kimataifa wa mabadiliko ya kidigitali utakaosaidia ufikiaji wa teknolojia kwa watu Duniani ili kufanikisha mpango wa maendeleo endelevu (SDGs).
Akifungua mkutano huo wa siku kumi ulioanza hii leo Juni 6 hadi Juni 16, 2022 katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, amekumbusha wajumbe dhumuni na uzingatiaji wa ajenda na kuhakikisha hakuna mtu anayeachwa nyuma katika kusaka maendeleo kwa wote.
“Zaidi ya theluthi moja ya wanadamu bado hawana uwezo wa kufikiwa na huduma ya intaneti ni jukumu lako katika mkutano huu wa mawasiliano kuandaa mpango kazi mpya ambao utawaleta karibu watu bilioni 3 ambao hawajaunganishwa katika jumuiya yetu ya kimataifa ya kidijitali kwa sababu tunavyosema tusimuache mtu nyuma, tunamaanisha kutomwacha mtu yeyote nje ya mtandao wa intaneti,” amesema Guterres.
Mbali na kuishukuru Rwanda kwa kuandaa mkutano huo, pia Katibu Mkuu huyo amekumbusha umuhimu wa mpango kazi wa Kigali utakaopitishwa, kuweka ubinadamu mbele na kutatua changamoto ya mgawanyo wa kidigitali katika jamii utakaochochea ongezeko la usawa.
“Pengo la kidigitali linachochea utofauti wa kijamii, kiuchumi na kijinsia katika maeneo yote kutoka mijini mpaka vijijini, kutoka kwenye elimu mpaka sekta ya afya, kutoka utotoni mpaka utu uzima na kwakuwa mkutano huu unawaleta watu pamoja ikiwemo wakuu wa nchi, makampuni binafsi, asasi za kiraia na wadau wengine ni sehemu nzuri ya kukubaliana masuala muhimu ikiwemo uwazi, uhuru na usalama katika mitandao ya kidijitali,” amefafanua Guterres.
Mkutano huu ambao hufanyika mara moja kila baada ya miaka minne unatoa wito wa kutumia uwezo ambao haujatumiwa wa teknolojia ya kidijitali, ili kuharakisha kufikiwa kwa malengo 17 ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa na ajenda ya ITU ya kuunganisha watu wote ifikapo mwaka 2030.
Aidha, unatoa fursa ya kipekee kwa jumuiya za kimataifa kuunda mikakati ya kijasiri na ya kibunifu ya kidijitali, ili kusaidia kuvunja vizuizi vya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Mkutano huo umeandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mawasiliano Duniani (ITU), na umewakutanisha zaidi ya wadau 1,200 wakiwemo wakuu wa nchi na serikali, mawaziri na wawakilishi wa vijana kutoka mataifa mbalimbali Duniani.