Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres ameisifu Serikali ya Tanzania kwa jitihada zake za kutafuta amani nchini Burundi.
Guterres ametoa pongezi hizo wakati aliposimama kwa muda katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam akitokea Kenya.
Aidha, Katibu Mkuu huyo mpya wa UN alisimama kwa ajili ya kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Augustine Mahiga.
Pamoja na mambo mengine Guterres ametumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Serikali kwa juhudi zake za kutafuta amani nchini Burundi kupitia kwa Msuluhishi wa mgogoro huo, Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.
“Tanzania imekuwa kinara wa amani Afrika na duniani na naipongeza kwa dhati katika jitihada zake inazozifanya za kutafuta amani ya Burundi na katika nchi nyingine za ukanda huu,” amesema Guterres.
Kwa upande wake, Balozi Mahiga amewasilisha kutoka kwa Rais John Magufuli kuhusiana na hatua iliyofikiwa ya usuluhishi wa mgogoro wa Burundi na ushiriki wa Tanzania katika vikosi vya Umoja wa Mataifa vya ulinzi wa Amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Mbali na kufanya ziara nchini Kenya, Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ametembelea Somalia na kukutana na Rais mpya wa nchi hiyo, Hassan Sheikh Mohamud, ambapo ameagiza Jumuiya ya Kimataifa kuchukua hatua kuepusha balaa la njaa nchini humo, kutokana na hali mbaya ya ukame.