Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amezitaka Israel na Hamas kusitisha mapigano ambayo yamekuwa yakisababisha umwagaji damu katika ukanda wa Gaza.
Kundi la Hamas limeonya kuwa litashambulia miji ya Israel ya Beersheba na Ashdod, ikiwa jeshi la Israel litaendeleza mashambulizi yake katika Ukanda wa Gaza.
Aidha, Israel imesema kuwa jeshi lake limeyashambulia maeneo zaidi ya 100 ya Hamas katika ukanda huo, ikijibu makombora yapatayo 370 yaliyorushwa na Hamas na kuanguka Kusini mwa Israel kuanzia jana jioni hadi alfajir ya leo.
Ghasia hizo mpya baina ya pande hizo mbili zimefuatia operesheni ya kijasusi ya Israel iliyomuua mmoja wa makamanda wa Hamas kilomita kadhaa ndani ya Ukanda wa Gaza juzi Jumapili.
Hata hivyo, Israel imeongeza kuwa operesheni hiyo iliyokwenda vibaya ililenga kukusanya taarifa tu lakini haikudhamiria kuua.
Katika mapigano yaliyofuata, ndege za Israel ziliua wanamgambo 7 wa Hamas, huku Hamas ikimuua mwanajeshi mmoja wa Israel.