Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ameendelea kuzungumzia sakata la kutajwa na mkuu wa mkoa wa  Dar es Salaam, Paul Makonda katika orodha ya watuhumiwa wa biashara ya dawa za kulevya hali iliyopelekea kuhojiwa na kupekuliwa.

Akizungumza jana kanisani kwake jijini Dar es Salaam, Askofu Gwajima alisema kuwa ingawa watu wengi wamekuwa wakiwasiliana naye wakimsihi amfungulie kesi mkuu huyo wa mkoa wa Dar es Salaam, yeye ataendelea na mpango wake wa kumshtaki kwa Rais John Magufuli na kwamba kama hataona matokeo atamwambia Mungu.

“Watu wananiuliza, nitamfungulia [Mkuu wa Mkoa] kesi? Mimi nawaambia nitamwambia Rais Magufuli kama nilivyosema, kama hakuna kitu kitakachofanyika basi nitamwambia Mungu aliye juu na majibu yatapatikana,” Askofu Gwajima ananukuliwa.

Katika hatua nyingine, Gwajima alieleza kushangazwa na kile alichokiita ongezeko kubwa la watu kanisani kwake katika kipindi cha wiki tatu. Kipindi hiki ni tangu alipotajwa na kuhojiwa na jeshi la polisi ambapo kwa mujibu wake hakupatikana na hatia yoyote kuhusu tuhuma za kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya.

Baada ya kunukuu vifungu kadhaa vya Biblia, Gwajima alieleza kuwa kilichomtokea yeye kilitokea kwa sababu na sio bahati mbaya na kwamba ili kufikia mafanikio kama yake ni lazima kuvumilia changamoto alizopitia katika maisha. Hii ni wiki ya pili mfululizo ambapo Gwajima amekuwa akizungumzia sakata hilo wakati wa ibada kanisani kwake.

Askofu huyo alitajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, kuwa kati ya 65 ya watuhumiwa wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya au matumizi ya dawa hizo.

Hata hivyo, baada ya kuhojiwa na kufanyiwa vipimo na mkemia mkuu wa Serikali kabla ya kupekuliwa nyumbani kwake, alieleza kuwa Jeshi la Polisi lilijiridhisha kuwa hahusiki na tuhuma hizo.

Video: Jaji Warioba ajitosa vita dawa za kulevya, Mawaziri 13 kikaangoni
Magazeti ya Tanzania leo Februari 27, 2017